May 03, 2012

Wazazi katika maisha yangu /Yetu.

Wazazi katika maisha yangu /Yetu.
Nachunguza maisha yangu nilipofikia na nilikotoka. Nachunguza pia mchango wa wazazi au walezi wangu ktk maisha niliyo nayo.
Baba na Mama au walezi wangu wamehangaika sana kunilea. Pengine wamefanya hivyo kwa sababu ya upendo waliokuwa nao kwangu mimi mtoto wao. Lakini nadhani lililo kubwa zaidi ni kwa sababu walinileta duniani na hivyo walikuwa na wajibu kunitimizia yote niliyostahili kupata katika malezi yangu.
Kwa ajili yangu walijinyima hata waliyostahili kuyapata ili mradi waone furaha na siha yangu nzuri. Kuna wakati wamekosana na majirani hata marafiki kwa ajili yangu.
Wamepata shida wakati wa kunilea, shida za kutembea mchana na usiku kwa ajili yangu, shida za kukosa hata usingizi wakati ninanyonya, kunihudumia wakati ninaumwa, kubembelezwa, na hata wakati nilipokuwa nalia bila sababu wao wamelia na mimi. Walinipa ulinzi kuhakikisha niko salama wakati wote. Kuna wakati wamejinyenyekeza mbele za watu kupata mikopo ya pesa ili walipe karo ya shule yangu. Wameniwezesha kusoma na hatimaye kupata elimu na ujuzi nilionao.
Nimepata kazi zenye kunipa kipato nilichonacho, nina uhakika wa kula na kunywa, wa kulala pazuri, kuoga maji safi na salama, kuvaa jinsi nipendavyo, kuburudika na kutengeneza maisha ya furaha.
Leo nimejiuliza sana ni zawadi gani nimewapa na wanafaidi nini kutoka kwangu? Hata kama bado wana nguvu na uwezo lakini nimewahi kuonyesha upendo na ishara za kuwakumbuka?
Matumizi mabaya ya fedha kupindukia, uhuni, burudani za kupita kiasi, fujo zote hizi nifanyazo za kujiona bora nk. vyote hivi navifanya nikikumbuka wao walivyojinyima kwa ajili yangu?
Ninapotumia laki tano, laki moja, hamsini elfu, ishirini elfu, kumi elfu, elfu tano, elfu tatu au kunywa bia moja, soda, juice au pipi, kuna sehemu ya chochote ninachowapa?
Ni kweli nahitaji kufanya maisha yangu nami yawe mazuri na yenye furaha na ya kuvutia kwa watu. Lakini je nahitaji kufanya hivi bila kuwakumbuka?
Je tangu mwaka uanze nimewapelekea chochote? Mwezi uliopita nimewatumia hata salamu? Je leo nimewakumbuka hata kuwaombea maisha marefu? Je mwishoni mwa mwezi huu ninayo plan yoyote ya kuwatumia chochote? Kama vile nguo za kuvaa? Mfano: - Shat moja kwa baba shilingi kama 15,000/= tu, pair ya khanga kwa mama shilingi 10,000/= au hata kwa ujumla kuwatumia shilingi 30,000/= tu kila baada ya miezi mitatu? Yaani shilingi 10,000/= kila mwezi. Nafanya hivi?
Kama sifanyi hivyo napaswa kupata muda wa ziada kupima matendo na mwenendo wangu.
Maana hata sasa nagundua kuwa nashindwa kueleza jinsi nilivyotumia mshahara wangu wa mwezi uliopita kwa ukamilifu. Nimepiga hesabu na kigundua kuwa kuna kiasi cha fedha tena nyingi zimepotepotea mikononi mwangu bila mimi kujua nimezitumia wapi. Na baadaye nimeona mwenyewe kwamba kweli ninachofanya si haki.
Ni baada ya kufikiria haya ndipo nikakumbuka kuwa sasa nina wajibu fulani kwa wazazi wangu.
wenzangu vipi???????????????

No comments: